20 Mei 2026
Kituo cha Afrika cha Masomo ya Kimkakati: FSB ya Urusi Inaendesha Mtandao wa Kibiashara wa Binadamu wa Bara Zima Kulisha Vita Vyake Ukraini

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Kituo cha Afrika cha Masomo ya Kimkakati, uliochapishwa Mei 19, 2026, umethibitisha kuwa Huduma ya Usalama wa Shirikisho la Urusi (FSB) inaendesha moja kwa moja mpango wa bara zima wa kuwapeleka raia wa Kiafrika katika majukumu ya mapigano na viwanda vya silaha kusaidia vita vya Moscow dhidi ya Ukraini. Kilichoanza kama ripoti za hapa na pale za udanganyifu wa uajiri kimethibitishwa kuwa ni operesheni ya kimfumo, inayoendeshwa na serikali.
Urusi inahitaji takriban waajiriwa wapya 30,000-35,000 kila mwezi ili kuziba upungufu wa askari waliopotea uwanjani kwenye mstari wa mbele wa kilomita 1,200 huku ikiepuka uhamasishaji wa jumla wa kitaifa unaobeba hatari kisiasa nyumbani. Makadirio yanaonyesha jumla ya vifo na majeruhi wa Kirusi ni takriban milioni 1.2 tangu 2022 - ikiwemo vifo vinavyoweza kufikia 325,000. Waafrika wanatumiwa kuziba pengo hilo.
Hifadhidata ya Kirusi iliyovuja ya waajiriwa wa Kiafrika kuanzia 2023 hadi 2025 inaonyesha mkakati wa makusudi wa kuzalisha wanajeshi wa mstari wa mashambulizi. Zaidi ya Waafrika 1,700 kutoka nchi 36 kwa sasa wamethibitishwa kupigana kwa ajili ya Urusi - lakini idadi hiyo huenda ikawa sehemu ndogo tu ya jumla. Ripoti ya kiintelijensia ya Kenya iliyowasilishwa Bungeni ilionyesha kuwa zaidi ya Wakenya 1,000 pekee walikuwa wameajiriwa - idadi ambayo ni asilimia 2,100 zaidi ya idadi inayoonekana kwenye hifadhidata iliyovuja.
Jinsi mtandao huo unavyofanya kazi
Uajiri unafuata mfumo thabiti katika bara zima. Vijana wa Kiafrika wanaahidiwa kazi za kiraia, fursa za michezo, mipango ya masomo, au hadhi halali ya kuishi Urusi. Wakishawasili, wanaonyeshwa mikataba iliyoandikwa kwa herufi za Kisiriliki, wanatishwa endapo watakataa kutia saini, na katika hali nyingi hati zao za kusafiria zinanyang'anywa - jambo linalozuia kabisa uwezekano wowote wa kurejea nyumbani. Nchini Kenya, mitandao ya uhalifu ilijifanya kuwa waajiri walioidhinishwa na serikali chini ya kaulimbiu ya "Kazi Majuu" (kazi ng'ambo), wakitoza wanaotafuta kazi ili kuwapangia nafasi nje ya nchi kabla ya kuwaelekeza kwa siri hadi eneo la vita la Urusi. Waajiriwa walibanwa kutuma ujumbe chanya nyumbani na kuwaajiri marafiki na familia katika mtandao huohuo.
Nchini Afrika Kusini, waajiriwa walidai kuwa Duduzile Zuma-Sambudla, binti wa Rais wa zamani Jacob Zuma, aliwadanganya kuamini kuwa watapewa mafunzo ya kuwa walinzi wa kibinafsi (bodyguards) nchini Urusi. Yeye na wengine wawili walilipwa, kulingana na ripoti, takriban dola 845,000 na Kundi la Wagner kwa kuwaelekeza raia wa Afrika Kusini kwenye vita hiyo. Zuma-Sambudla alijiuzulu kiti chake cha Bunge mwezi Desemba 2025 baada ya ufichuzi huo na uchunguzi wa polisi.
Unyonyaji wa Urusi unaenea zaidi ya mahandaki. Uchunguzi umethibitisha mamia ya waajiriwa wa Kiafrika - hasa wanawake vijana - wanaofanya kazi chini ya mipango ya udanganyifu ya "kazi-masomo" katika vituo kama vile kiwanda cha ndege zisizo na rubani cha Alabuga [tata la utengenezaji wa silaha huko Tatarstan - Mhariri], takriban kilomita 1,000 mashariki mwa Moscow. Waajiriwa walioahidiwa mafunzo ya usimamizi wa vifaa (logistics) na ukarimu (hospitality) badala yake wanalazimishwa kutengeneza silaha chini ya hali hatari na za kulazimishwa, wakipokea sehemu ndogo tu ya mshahara walioahidiwa bila njia dhahiri ya kurejea nyumbani. Inakadiriwa mtandao huo unahusisha zaidi ya Waafrika 1,000.
Kinachotokea mstari wa mbele
Waajiriwa wa Kiafrika wanapangiwa kwa makusudi majukumu ya uwanjani yanayoweza kutupwa kirahisi. Wanasukumwa kuelekea nafasi za mstari wa mbele wakiwa na mafunzo kidogo, vifaa duni, na ugavi mdogo. "Tulikuwa chakula cha mizinga. Baadhi yetu hatukuwa hata tunajua kufyatua risasi vizuri kabla hawajatusukuma mbele," alisema Mwafrika Kusini mmoja aliyekuwa amedanganywa kuamini kuwa anasafiri kwenda Urusi kufanya kazi ya ulinzi wa kibinafsi. Katika video inayosambaa, askari wa Kirusi wanawadhihaki waajiriwa wa Kikenya kuwaita "wale wa kutupwa."
Athari kwa binadamu imeandikwa kwenye takwimu. Hifadhidata ya Kirusi iliyovuja inaonyesha kiwango cha vifo kilichothibitishwa cha asilimia 22 miongoni mwa Waafrika walioajiriwa. Kwa upande mwingine, uchambuzi unaonyesha asilimia 42 ya wapiganaji wa kigeni hufa ndani ya miezi minne baada ya kujiunga na Jeshi la Urusi. Nchi zenye idadi kubwa zaidi ya vifo vilivyothibitishwa ni pamoja na Cameroon (waliouawa 94), Ghana (55 kati ya 272 walioajiriwa), na Misri (52).
Ushuhuda kutoka kwa waliorejea unaeleza ukataji wa viungo, majeraha makubwa, hati zilizonyang'anywa, mishahara iliyozuiliwa, na unyanyasaji wa kibaguzi. Mwafrika Kusini mmoja aliyerejea alisema: "Walitufanya tuchome kila kitu tulichokuwa nacho - nguo, hati, hata picha za familia. Tangu mwanzo, ilikuwa jehanamu." Wakati mwajiriwa mmoja wa Kiafrika aliyejeruhiwa asiye na miguu alipouliza kama anaweza kurejea nyumbani, aliambiwa: "Mkataba wako utakapoisha."
Jibu la Kremlin kuhusiana na wingi mkubwa wa ushahidi, lililotolewa na msemaji Dmitry Peskov mwezi Mei 2026: "Hatujui kuhusu kesi zozote za aina hiyo."
Yanayofanyika
Serikali za Kiafrika zinazidi kudai uwajibikaji. Vyombo vya usalama vya Kenya vimevamia ofisi za mitandao ya uajiri na kuokoa watu 22 waliokuwa wakielekea Urusi katika operesheni moja. Kesi za jinai zimefunguliwa dhidi ya waajiri. Interpol imezindua uchunguzi nchini Botswana kuhusu uajiri wa kiwanda cha Alabuga. Kiongozi wa Wengi wa Bunge la Kitaifa la Kenya alionya kuwa mtandao huo wa biashara haramu ya binadamu tayari ulikuwa umebadilisha njia zake - kutoka Istanbul na Abu Dhabi kwenda kusafirisha waathirika kupitia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Uganda, na Afrika Kusini ili kuepuka kugunduliwa, huku kukiwa na ushahidi wa ushirikiano wa kificho ndani ya idara za serikali ya Kenya.
Kama kiongozi mmoja wa asasi za kiraia wa Ghana alivyosema: "Hali hii ni mchanganyiko wa upotoshaji wa habari, biashara haramu ya binadamu, na uingiliaji wa kigeni. Hii inahitaji mwitikio ulioratibiwa katika ngazi ya kikanda."
Mradi wa "Nataka Kuishi" (I Want to Live), ambao hifadhidata yake ndiyo msingi wa sehemu kubwa ya utafiti wa kiasi katika ripoti hii, unawasihi raia wote wa Kiafrika kukataa ofa zozote za ajira au huduma ya kijeshi zinazohusiana na Urusi na kuripoti shughuli za uajiri zinazotia shaka kwa mamlaka za kitaifa mara moja.